Kupanga uzazi, ujauzito na ufuatiliaji wa watoto
Kupanga uzazi
Kupanga uzazi
Wanasiasa nchini Norwei wanajadili jinsi wanavyoweza kuwahimiza wanandoa kupata watoto zaidi. Katika nchi zingine, wanawake wamewekewa vizuizi vikali kuhusu idadi ya watoto wanaoruhusiwa kupata. Katika baadhi ya mataifa, wanawake hupata watoto watano kwa wastani.
Kupanga uzazi kunamaanisha kuwa wanandoa wanaweza kubaini wakati haswa wanapotaka mwanamke awe mjamzito, na wangependa kuwa na watoto wangapi. Kupanga uzazi kunamaanisha kuzuia kupata mimba bila kutaka. Njia tofauti za kuzuia ujauzito zinaweza kuzuia hili lisitokee.
Mbinu za kawaida za kuzuia ujauzito ni:
- Tembe za kupanga uzazi ni vidonge vilivyo na homoni za estrojeni na jestageni/projesteroni. Tembe hizi huzuia udondoshaji wa kijiyai kwenye ovari.
- Kidude cha kupanga uzazi ni kijiplastiki kidogo kinachochomekwa chini ya ngozi. Kina homoni ya jestageni na huachilia kiasi kidogo kila siku. Homoni hii huzuia udondoshaji wa kijiyai kwenye ovari. Kijiplastiki hiki cha kupanga uzazi kinapaswa kuingizwa na kutolewa na daktari.
- Kitanzi cha kupanga uzazi huingizwa na daktari kwenye tumbo la uzazi la mwanamke. Kitanzi huzuia mzunguko wa mbegu za kiume na huzuia yai lolote lililotungishwa dhidi ya kupachikwa kwenye ukuta wa tumbo la uzazi.
- Kondomu ndiyo njia ya pekee ya kuzuia ujauzito inayomlinda mtu dhidi ya magonjwa ya zinaa. Pia ndiyo njia ya pekee ya kuzuia ujauzito inayotumiwa na wanaume. Inapendekezwa kutumia kondomu pamoja na mafuta ya kudhibiti mbegu za kiume ili kupunguza hatari ya kupata ujauzito bila kukusudia. Mafuta ya kudhibiti mbegu za kiume haizuii ujauzito inapotumika peke yake.
Kuchunguza ujauzito na kujifungua
Wanawake wajawazito nchini Norwe wana haki ya kupata huduma ya utunzaji wa ujauzito, bila malipo. Uchunguzi hufanywa katika vituo vya afya au na daktari wa kawaida wa mwanamke. Uchunguzi ni wa hiari, na husaidia kulinda afya ya mama na mtoto wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaa na baada ya kuzaa. Nchini Norwe, inapendekezwa wanawake wajawazito wamwone daktari kati ya mara 8-12. Wanawake wengi hujifungulia hospitalini, bila malipo.
Ukaguzi wa afya na chanjo
Watoto na vijana wote wanaoishi Norwe hufanyiwa ukaguzi wa afya mara kwa mara. Ukaguzi huu wa afya hufanyika katika vituo vya afya kuanzia wakati watoto wanapozaliwa hadi wanapoanza shule. Huduma ya afya kwa shule inawajibikia ukaguzi wa afya kwa watoto waliofika umri wa kwenda shule. Manispaa nyingi pia zina vituo vya afya vilivyotengewa vijana. Watoto na vijana wote wanaoishi Norwe hupewa chanjo dhidi ya magonjwa sugu. Chanjo hutoa kinga madhubuti, bora na salama dhidi ya magonjwa. Huduma kwenye vituo vya afya na huduma ya afya kwa shule zinatolewa bila malipo.
Daktari wa kawaida huchunguza kisha anamtibu mtoto ikiwa ni mgonjwa.
Kutoa mimba
Nchini Norwe, Sheria inayohusu Kutoa Mimba (Sheria ya Utoaji Mimba) inasema kuwa wanawake wanaruhusiwa kutoa mimba ndani ya wiki 12 za kwanza za ujauzito. Mwanamke sharti ajaze na kuwasilisha fomu inayothibitisha kuwa angependa kutoa mimba na kwamba anafahamu masuala ya matibabu yanayohusiana na utoaji mimba na kuhusu uwezekano wa kupata maelezo zaidi kuhusu njia mbadala za kutoa mimba. Sheria ya Utoaji Mimba pia inabainisha kinachopaswa kufanyika endapo mwanamke angependa kutoa mimba baada ya wiki ya kumi na mbili ya ujauzito.
Jadilianeni pamoja
- Je, suala la kupanga uzazi linachukulia vipi katika nchi unazojua? Je, ni kawaida kwa watu kutumia mbinu za kuzuia ujauzito?
- Je, kwa nini uchunguzi wa ujauzito unachukuliwa kuwa muhimu sana hivi kwamba huduma hii inatolewa bila malipo?
- Je, kwa nini ni muhimu kwa wazazi kukubali huduma zinazotolewa na vituo vya afya?
- Je, unafikiria nini juu ya ukweli kwamba watoto wengi nchini Norway wamepewa chanjo dhidi ya magonjwa kadhaa?
- Je, kwa nini watoto wanapewa chanjo bila malipo?
Jadili kauli:
- Sheria ya utoaji mimba inahusisha haki ya wanawake kujiamulia na ulinzi wa kisheria wa mtoto aliye tumboni.
Chagua jibu sahihi
Kwa wastani, wanawake Wanorwe huzaa watoto wangapi?
Chagua jibu sahihi
Je, nini maana ya kupanga uzazi? Unaweza kuchagua zaidi ya jibu moja.
Chagua jibu sahihi
Je, kituo cha afya kina jukumu gani?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?