Wajibu na haki za kidemokrasia
Wajibu na haki za kidemokrasia
Watu wanaoishi katika nchi ya demokrasia wana uhuru, wajibu, haki na majukumu. Tutaangalia kwanza haki muhimu zaidi.
Haki za binadamu
Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu lilipitishwa mnamo 1948.
Usawa
Kila mtu ana haki na fursa sawa bila kujali umri, kabila, uwezo, jinsia, dini na mwelekeo wa kingono.
Uhuru wa kujieleza
Uhuru wa kujieleza inamaanisha kuweza kutoa maoni yako kuhusu siasa, dini na mambo mengine, kujadili na wengine na kuandika kwa uwazi kuhusu misimamo yako bila kuadhibiwa. Tuna sheria zinazoweka mipaka kwa uhuru wa kujieleza. Kwa mfano, watu hawaruhusiwi kutoa kauli zinazoonyesha ubaguzi na kueneza chuki, iwe kwa maneno au kupitia maandishi. Uhuru wa kujieleza unatumika kwa watu binafsi na kwa vituo vya redio na televisheni na magazeti.
Haki ya kupiga kura
Katika demokrasia, watu wana haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa kisiasa. Umri wa kupiga kura nchini Norwe ni miaka 18. Uchaguzi nchini Norwe unafanyika kupitia kura ya siri. Hii inamaanisha kuwa watu wengine hawajui uliyempigia kura. Sharti uwe raia wa Norwe ili uweze kupiga kura katika uchaguzi mkuu. Ili uweze kupiga kura katika uchaguzi wa mabaraza ya kaunti na manispaa, sharti uwe umeishi Norwe kwa miaka mitatu kabla ya uchaguzi.
Kulindwa kisheria
Kulindwa kisheria, au utawala wa sheria, unamaanisha, miongoni mwa mambo mengine, kwamba huwezi kuhukumiwa bila ya kesi kusikilizwa. Katika nchi ya kidemokrasia, kesi inamaanisha kwamba hakimu huru ndiye anayeamua ikiwa mshtakiwa ana hatia au hana, na kuwa hakimu huru ndiye anayeamua adhabu ikiwa mshtakiwa atapatikana na hatia. Washtakiwa wote wana haki ya kujitetea.
Uhuru wa kidini na imani
Uhuru wa kidini na imani unamaanisha kuwa watu wana uhuru wa kuchagua dini yoyote au kushikilia msimamo wowote wanaotaka, na kwamba wako huru kufuata dini au misimamo yao. Yaani, hakuna mtu aliye na haki ya kuwalazimisha wengine kujiunga au kuacha dini fulani. Hakuna atakayenyanyaswa au kuadhibiwa kwa sababu ya dini yake. Kuanzia umri wa miaka 15, kila mtu ana haki ya kujiunga au kuacha dini au jumuiya fulani kwa hiari yake, bila kujali maoni ya wengine. Kuwa na uhuru wa kuchagua kutoshiriki katika dini au jumuiya fulani ni muhimu sawa na kuwa huru kuchagua dini au jumuiya.
Uhuru wa kutangamana
Uhuru wa kutangamana unamaanisha mambo kadhaa. Hizi ni baadhi ya maana muhimu zaidi:
- Watu wana haki ya kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa au vyama vingine bila kunyanyaswa au kuadhibiwa.
- Watu wana haki ya kuwa wanachama wa chama cha wafanyakazi bila kunyanyaswa au kuadhibiwa. Katika hali fulani, watu pia wana haki ya kugoma.
- Watu wana haki ya kutoa malalamishi yao katika maandamano halali.
Haki na wajibu
Kama tunavyoona, watu wanaoishi katika nchi ya kidemokrasia wana haki nyingi. Uhuru huu na haki hizi huambatana na wajibu na majukumu. Sharti tuzingatie sheria na kanuni zilizowekwa na walio wengi. Tuna haki ya kujaribu kubadilisha mambo tusiyoyapenda katika jamii, lakini sharti tuzingatie kanuni za demokrasia. Jamii ya Norwe kwa kiasi kikubwa inategemea kuaminiana. Hii inamaanisha kuwa maafisa wa serikali wanatarajia wananchi kutoa taarifa ya kweli na kuzingatia sheria na kanuni, nao wananchi wana imani kuwa watahudumiwa inavyofaa k.m. na polisi au huduma za maslahi ya watoto.
Je, ni nini kinachoweza kutishia demokrasia?
Vipengele hivi vinaweza kuwa vitisho kwa demokrasia:
Idadi ndogo ya wanaojitokeza kwenye uchaguzi.
Imani iliyopungua kwa wanasiasa.
Habari za uwongo na matamshi ya chuki ambayo yanasimamisha mjadala wazi kwa umma.
Migogoro mikuu ya kitaifa ambayo inafanya iwe muhimu kukwepa michakato ya kidemokrasia.
Sheria na kanuni zinazotumika kwa nchi kadhaa huchukua nafasi ya kwanza kuliko sheria za nchi zilizotungwa kwa njia ya kidemokrasia.
Jadilianeni pamoja
- Je, maisha yako vipi katika nchi ya kidemokrasia?
- Je, maisha yako vipi katika nchi isiyo ya kidemokrasia?
- Jadili kuhusu wajibu unaodhani unaambatana na haki katika nchi ya kidemokrasia.
- Je, unajua wajibu na haki zipi za kidemokrasia?
- Jadili kwa nini idadi ndogo ya wanaojitokeza kwenye uchaguzi na imani iliyopungua kwa wanasiasa ni tishio kwa demokrasia.
- Je, ni kwa njia gani uaminifu ni kipengele muhimu cha jamii ya Norway? Je, unayo mifano ya jinsi hii inavyoelezwa?
Chagua jibu sahihi
Je, kuna uhuru kamili wa kujieleza nchini Norwe?
Chagua jibu sahihi
Je, umri wa kupiga kura ni upi nchini Norwe?
Chagua jibu sahihi
Je, ni nani ana haki ya kujitetea akishtakiwa kwa kosa la uhalifu?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?