Demokrasia nchini Norwe
Tazama filamu
Demokrasia nchini Norwe
Serikali kuu, mamlaka za kaunti na manispaa
- Kuna kaunti 15 na manispaa 356 nchini Norwe (1.01.2024).
- Kaunti na manispaa ni maeneo ya kijiografia na ni vitengo vya utawala vinavyoongozwa na viongozi wa kisiasa.
- Mamlaka za kaunti na manispaa zinajitawala katika masuala fulani, ingawa serikali kuu husimamia mambo mengi.
- Serikali kuu huweka mfumo unaotumiwa na kaunti na manispaa.
- Serikali kuu inatawala nchi nzima, nazo mamlaka za kaunti na manispaa husimamia masuala ya ndani pekee.
Baadhi ya majukumu ya serikali kuu ni:
- sera za kigeni
- hospitali
- sheria
- mitaala ya shule
Baadhi ya majukumu ya mamlaka za kaunti ni:
- shule za sekondari
- barabara za kaunti
Baadhi ya majukumu ya manispaa ni:
- shule za msingi na sekondari
- shule za chekechea
- kuwatunza wakongwe
- kukusanya takataka, maji na maji taka
- barabara za manispaa
Udhibiti wa kisiasa na kiutawala
Serikali kuu, kaunti na manispaa zinatawaliwa na wanasiasa waliochaguliwa na wananchi. Hii inamaanisha kuwa wanasiasa hujadili masuala na kubuni sera za maeneo tofauti. Hata hivyo, ni watumishi wa umma katika usimamizi wa umma – serikali, mamlaka za kaunti na wafanyakazi wa manispaa – ambao hutekeleza sera.
Mifano:
- Wanasiasa hupitisha mitaala ya masomo. Walimu hufundisha kwa kufuata mitaala hii.
- Wanasiasa hupitisha sheria za malipo ya faida za ustawi wa jamii. Wafanyakazi wa NAV sharti wazingatie sheria hizi.
Bunge
Bunge la Norwe linajulikana kama Storting. Lina wabunge 169 waliochaguliwa na wananchi kuhudumu kipindi cha miaka minne. Wabunge wanawakilisha vyama tofauti vya siasa. Bunge ndiyo tawi kuu zaidi ya serikali nchini Norwe.
Majukumu muhimu zaidi ya bunge ni:
- kupitisha sheria mpya na kurekebisha zile za zamani
- kuidhinisha bajeti ya kitaifa
- kusimamia masuala ya serikali na utawala wa serikali kuu
- kujadili masuala ya kisiasa na miradi mikubwa
Norwe ina demokrasia huru. Mtu yeyote anaweza kuhudhuria vikao vya Bunge ili kuwasikiliza wanasiasa wakijadili masuala mbalimbali. Hata hivyo, ukiwa katika bunge huna haki ya kuzungumzia au kutoa kauli kuhusu masuala. Masuala mengi yanasambazwa kwa ajili ya mashauriano. Hii inawapa wataalam na watu wa kawaida nafasi ya kutoa maoni yao.
Serikali
Baada ya uchaguzi mkuu, chama kimoja au kadhaa huunda serikali mpya. Serikali inajumuisha mawaziri (wakuu wa kisiasa wa kila wizara) na waziri mkuu. Mojawapo ya majukumu ya serikali ni kupendekeza sheria mpya na kurekebisha sheria zilizopo, lakini Bunge ndilo hupitisha sheria na marekebisho ya sheria. Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa na Bunge yanatekelezwa. Serikali pia huandaa bajeti ya kitaifa kila mwaka.
Baraza Kuu
Serikali huwa na mkutano na Mfalme kila Ijumaa. Katika mikutano hii, mawaziri humjulisha Mfalme kuhusu masuala tofauti ya kisiasa. Mkutano huu unajulikana kama Baraza Kuu. Ingawa mfalme hana mamlaka ya kisiasa, mikutano hii ni muhimu.
Kugawanya mamlaka
Kugawanya mamlaka inamaanisha kuwa tawi tatu huru za serikali zina mamlaka ya kujisimamia.
- Tawi la Bunge hupitisha sheria.
- Tawi la serikali hupendekeza sheria na kuhakikisha zinatekelezwa.
- Tawi la mahakama (korti) hutoa uamuzi katika kesi zinazosikilizwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizoidhinishwa na Bunge.
Kwa kugawanya mamlaka kati ya tawi hizi tatu za serikali, hakuna tawi litakalokuwa na mamlaka kupita kiasi. Hivyo hii inadumisha demokrasia.
Jadilianeni pamoja
- Jadili kuhusu idara za serikali katika nchi unazojua.
- Jadili kuhusu ugawanyaji wa mamlaka nchini Norwe.
- Jadili majukumu ya serikali kuu, kaunti na manispaa katika jamii ambapo maslahi ya watu yanazingatiwa.
- Je, unawezaje kuchangia katika masuala ya jamii unakoishi?
- Je, unadhani ni rahisi kuchangia katika masuala ya kieneo kuliko ya kitaifa? Je, kwa nini ni rahisi au si rahihi?
Chagua jibu sahihi
Je, lipi ni jukumu la serikali kuu?
Chagua jibu sahihi
Je, Bunge la Norwe linaitwaje?
Chagua jibu sahihi
Je, waziri ni nani?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?