Shule ya upili na elimu ya juu
Tazama filamu
Shule ya upili
Kazi nyingi zinahitaji uwe umefika shule ya upili au kiwango cha elimu ya juu. Hivyo basi, watu wengi huamua kuendelea na masomo baada ya shule ya kati.
- Wanafunzi ambao wamemaliza shule ya msingi wana haki ya kupata nafasi katika shule ya sekondari ya juu.
- Haki ya kupata elimu ya sekondari ya juu hudumu hadi uwe umefanikisha uwezo wako wa kielimu au ufundi.
- Wanafunzi hawalipi karo katika shule za upili za umma.
- Wanafunzi huchagua kati ya masomo ya jumla na ya kiufundi.
- Wanafunzi sharti wawasilishe ombi la kujiunga na shule ya upili kabla ya tarehe 1 Machi, na wanapaswa kuwasilisha ombi hili mtandaoni.
- Alama wanazopata katika darasa la 10 hubaini shule ya upili watakayosomea.
- Kuna shule za upili za kibinafsi. Wanafunzi wanaokwenda kusomea shule za upili za kibinafsi hulipa karo.
Masomo ya Kiufundi: Wanafunzi wanapata elimu ya utendaji na wanapokea cheti cha ufundi wanapomaliza masomo yao. Mifano ya elimu ya utendaji ni pamoja na useremala, ususi, uhudumu wa afya na ufundi wa magari.
Masomo ya jumla: Wanafunzi wanapata elimu ya kinadharia. Wanafunzi walio na cheti kutoka kwa mpango wa masomo ya jumla wanaweza kuwasilisha ombi la kujiunga na chuo au chuo kikuu.
Mtandao
Chanzo: SSB (Ofisi ya Takwimu ya Norway)
Elimu ya juu
Jamii ya kisasa inayozingatia maslahi ya watu wake inategemea ajira, teknolojia, uzalishaji na uvumbuzi. Kwa hivyo Norwe inahitaji watu waliosoma sana. Mamlaka za umma husaidia kuhakikisha hili, kwa mfano kwa kutoa nafasi sawa za elimu kwa watu wote.
Karibu asilimia thelathini na tano ya watu wazima nchini Norwe wana elimu ya juu. Vijana zaidi wanafikia kiwango cha elimu ya juu, na kiwango hiki cha elimu nchini Norwe kinakua kwa kasi. Kwa sasa, zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi ni wanawake na wana kiwango cha juu kidogo cha elimu kuliko wanaume. Ikilinganishwa na idadi ya watu kwa jumla, waliozaliwa na wazazi wahamiaji nchini Norwe ni wengi zaidi katika elimu ya juu.
Kila mtu ambaye amefuzu kujiunga na elimu ya juu kutoka shule ya upili anaweza kuomba nafasi katika chuo au chuo kikuu.
- Wanafunzi hawalipi karo katika vyuo na vyuo vikuu vya umma, lakini wanalipia vitabu vyao.
- Tume ya Usajili wa Wanafunzi katika Vyuo na Vyuo Vikuu inasimamia usajili kwa niaba ya vyuo na vyuo vikuu. Taarifa kuhusu tarehe za mwisho za kutuma maombi zinapatikana kwenye tovuti.
Mtandao
Mkopo wa Serikali wa Kufadhili Elimu (Lånekassen)
Ingawa wanafunzi hawalipi karo katika vyuo na vyuo vikuu, wanahitaji pesa kushughulikia gharama zingine wanapoendelea na masomo. Hivyo ni kawaida kwa wanafunzi kukopa pesa kupitia Mkopo wa Serikali wa Kufadhili Elimu ili kulipia kodi ya nyumba, chakula na mahitaji mengine. Mkopo wa Serikali wa Kufadhili Elimu hutoa mikopo na usaidizi wa kifedha kwa wanafunzi nchini Norwe na kwa wanafunzi wa Norwe wanaosoma nchi za nje. Hii inahakikisha kuwa kila mtu anayetaka kufikia elimu ya juu anaweza kufanya hivyo bila kujali jinsia, umri, hali ya kijamii na hali ya kifedha ya familia zao. Watu wazima wanaweza pia kuomba mikopo na/usaidizi wa kifedha ili kulipia elimu ya msingi au upili.
Mikopo inapaswa kulipwa kila mwezi baada ya kumaliza masomo. Huhitaji kulipa pesa ulizopokea kupitia ufadhili, lakini mara nyingi ufadhili hujumuisha masharti kwamba wanafunzi wakamilishe masomo na wafaulu katika mtihani wao.
Jadilianeni pamoja
- Vijana na watu wazima waliomaliza elimu ya msingi wana haki ya kupata elimu ya sekondari ya juu. Hii inasema nini kuhusu jamii? Inatuambia nini kuhusu matarajio katika maisha ya kazi?
- Watu zaidi nchini Norwe wanazidi kupata elimu ya juu. Je, hii inonyesha nini kuhusu matarajio ya wafanyakazi na fursa za kazi nchini Norwe?
- Mkopo wa Serikali wa Kufadhili Elimu ulianzishwa mnamo 1947. Ilikuwa kuwezesha watu wote kupata elimu ya juu, bila kujali asili. Mkopo wa Serikali wa Kufadhili Elimu ni benki na ni sehemu muhimu ya ustawi wa jamii. Je, maoni yako ni yapi kuhusu mpango huo?
Chagua jibu sahihi
Je, elimu ya kiufundi ni nini?
Chagua jibu sahihi
Je, kuna shule za upili za kibinafsi nchini Norwe?
Chagua jibu sahihi
Je, watu wazima ni wangapi nchini Norway walio na elimu ya juu?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua picha sahihi
Je, ni picha ipi inayoonyesha elimu ya kinadharia?