Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia
Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia
Norwe ikawa nchi huru tena mnamo 1905. Mwamko mpya. Idadi ya watu iliongezeka mwanzoni mwa miaka ya 1900, watu walihamia mijini na viwanda vikapanuka.
Norwe ina maporomoko mengi ya maji, na watu walianza kutumia maji kuzalisha umeme mwishoni mwa karne ya 19. Viwanda vingi vilifunguliwa, na wafanyakazi walihitajika kwa wingi. Watu wengi walihamia mijini. Umeme uliwekwa katika nyumba zingine, taa za barabarani zililetwa katika miji na treni ya umeme ikaanza kutumika katika baadhi ya miji. Injini za dizeli zilitumika kwenye meli, hivyo kuziwezesha kusafiri mbali na kwa haraka zaidi. Magari ya kwanza yalifika Norwe.
Sheria maalum ilihakikisha kuwa watu binafsi wanaweza kuzalisha umeme unaotokana na maji, lakini umeme wenyewe unabaki kuwa mali ya umma.
Hiki kilikuwa kipindi cha shughuli nyingi kwenye Bunge la Norwe. Vyama vya wafanyakazi vilitetea maslahi ya wafanyakazi na vilitumia shinikizo ili kuleta mabadiliko. Bunge lilipitisha sheria nyingi mpya, ikiwemo kuruhusu tu watu kufanya kazi saa kumi kwa siku. Saa hizi za kazi zilipunguzwa hadi nane mnamo 1919. Wafanyakazi wote walikuwa na haki ya kufidiwa kutokana na ugonjwa, hii inamaanisha kuwa walipokea pesa kutoka kwa serikali kuu walipougua.
Wanaume zaidi ya umri wa miaka 25 walikuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu kuanzia mwaka wa 1898, na wanawake walio zaidi ya miaka 25 walipata haki hiyo mnamo 1913.
Vita vya Kwanza vya Dunia
Vita vya Kwanza vya Dunia viliendelea Ulaya katika miaka ya 1914-1918. Norwe haikushiriki katika vita, lakini athari za kiuchumi zilizotokana na vita ziliiathiri. Vita hivi vilisababisha upungufu wa bidhaa kama vile nafaka, kahawa na sukari, na bidhaa hizi zilidhibitiwa.
Miaka kati ya vita viwili
Kipindi kati ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia kinajulikana kama miaka kati ya vita viwili Katika sehemu nyingi ulimwenguni, karibu kipindi hiki chote kilikuwa na matatizo ya kifedha nchini Norwe. Watu wengi hawakuwa na ajira.
Vita vya Pili vya Dunia
Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya Wajerumani kuvamia Polandi mnamo Septemba 1939. Utawala wa Norwe ulichukuliwa na vikosi vya Wajerumani mnamo tarehe 9 Aprili 1940. Vita nchini Norwe vilidumu kwa wiki chache kabla ya Norwe kujisalimisha. Mfalme na Wakuu wa Serikali walikimbilia Uingereza na kuendelea na mapambano ya kuikomboa Norwe wakiwa huko. Norwe ilitawaliwa na serikali ya Wajerumani iliyoongozwa na Vidkun Quisling. Serikali hii haikuchaguliwa kidemokrasia.
Ingawa mapigano madogo yalifanyika nchini Norwe, vikundi kadhaa vya upinzani vilifanya hujuma, vilichapisha magazeti haramu na kuandaa uasi wa kiraia na upinzani usio dhahiri dhidi ya vikosi vya wanajeshi wa Ujerumani. Watu wengi ambao walishiriki katika harakati za upinzani walilazimika kutorokea nchi nyingine. Takriban Wanorwe 50,000 walikimbilia Uswidi wakati wa vita. Wengi wao walijiweka katika hatari kubwa ili kusaidia wengine.
Kaskazini mwa Norwe, watu wengi waliuawa na sehemu nyingi za kaunti ya Finnmark na sehemu ya kaskazini ya kaunti ya Troms ziliteketezwa wakati majeshi ya Ujerumani yalipoondoka maeneo haya. Kwa amri ya Hitler, majengo na miundombinu nyingi ziliteketezwa kwa moto.
Mwishowe, Ujerumani ilianza kushindwa vita sehemu mbalimbali, na ililazimika kujisalimisha mnamo Mei 1945. Zaidi ya Wanorwe 10,000 walifariki kutokana na vita.
Kabla ya vita, idadi ya Wayahudi nchini Norwe ilikuwa karibu watu 2,100. Kati ya idadi hii, 773 walipelekwa kwenye kambi za mateso, na 38 pekee ndio walinusurika na kurejea Norwe baada ya vita.
Jadilianeni pamoja
- Je, unadhani ni kwanini Bunge lilipitisha sheria zilizofanya maisha yawe rahisi kwa wafanyakazi?
- Je, Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia vilikuwa vipi katika nchi yako?
- Jadilianeni pamoja kuhusu jinsi vita vinavyoathiri jamii na watu wanaoishi huko.
Je, haki za binadamu hushughulikiwa vipi wakati wa vita?
Chagua jibu sahihi
Je, wanawake walipata lini haki ya kushiriki katika uchaguzi nchini Norwe?
Chagua jibu sahihi
Je, kipindi cha kati ya vita viwili kilikuwa lini?
Chagua jibu sahihi
Je, majeshi ya Ujerumani yaliingia lini Norwe?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Bofya picha
Bofya mwaka sahihi. Je, Vita vya Pili vya Dunia vilikuwa lini?