Afya na mtindo wa maisha
Tazama filamu
Afya na mtindo wa maisha
Matukio ya Kihistoria
Hali ya maisha iko juu nchini Norwe hivi leo. Dawa za magonjwa mengi sugu zinapatikana, na nchi hii inayozingatia maslahi ina mifumo ya kuhakikisha kuwa dawa na huduma za kimatibabu zinapatikana kwa watu wote. Watoto wanapewa chanjo za bila malipo dhidi ya magonjwa mbalimbali. Watu wengi walikuwa wakifa nchini Norwe kutokana na magonjwa yanayohusiana na umaskini, k.m. utapiamlo na kifua kikuu. Watu wengi pia walikufa kutokana na ukosefu wa matibabu.
Hali ya afya ya umma nchini Norwe imeimarika sana katika kipindi cha miaka 100 iliyopita. Hii ni kutokana na uzingatiaji wa maslahi ya wakaazi, ambao hutoa fursa zaidi na bora za kuishi maisha mazuri na salama. Watu nchini Norwe wanaishi maisha marefu kuliko hapo awali. Wakongwe wengi pia wana afya ikilinganishwa na hapo awali. Hii inawawezesha kuishi maisha marefu, mazuri na wanaweza kuendeleza shughuli mbalimbali.
Hii haimaanishi kuwa hakuna magonjwa nchini Norwe. Kwa mfano, watu wengi wanakabiliwa na matatizo ya misuli na mifupa. Ugonjwa wa kisukari na kunenepa kupita kiasi pia zinaongezeka. Magonjwa ya moyo na mishipa, pamoja na saratani, ndio sababu kuu za vifo nchini Norwe.
Kuzuia matatizo ya kiafya
Hali ya afya yetu mara nyingi huhusishwa na mtindo wetu wa maisha. Hii inahusisha afya yetu ya mwili na akili. Tukila lishe bora na tufanye mazoezi ya mwili, tutaishi kuwa wenye afya kwa muda mrefu. Watu wanaovuta sigara wako katika hatari kubwa ya kupata saratani na magonjwa ya moyo na mishipa.
Japo serikali huwajibika pakubwa katika kulinda afya ya umma, ni wajibu wa mtu binafsi pia kuzingatia anavyoishi na anavyotunza afya yake.
Afya ya akili ni muhimu sawa na afya ya mwili. Watu wengi hufurahia kuingiliana na watu wengine. Hii inaweza kuwa kupitia familia, kuwa na marafiki au wafanyakazi-wenza. Kuwaza mazuri, kuwa na utulivu, kulala vyema na kufurahia pia ni muhimu kwa afya yetu. Kuna msemo wa Kinorwe unaosema kuwa kucheka hurefusha maisha.
Lishe
- Jadili uhusiano uliopo kati ya lishe na afya.
- Je, vyakula unavyokula sasa ni sawa na ulivyokuwa ukila kabla ya kuja Norwe?
- Je, upo uhusiano kati ya hali ya hewa na lishe?
- Je, unadhani ni vyakula gani vina madhara mwilini?
- Je, unadhani ni vyakula gani vina afya?
Wahudumu wengi wa afya wanaotangamana na wahamiaji wana wasiwasi kuhusu afya zao. Wana wasiwasi kwa sababu, ikilinganishwa na Wanorwe, wahamiaji wengi wana matatizo yafuatayo, kati ya mengine:
- ugonjwa wa kisukari
- kunenepa kupita kiasi
- matatizo ya meno
- utapiamlo, haswa ukosefu wa madini na vitamini D
- msongo wa mawazo
Jadilianeni pamoja
ugonjwa wa kisukari – saratani – pumu – kunenepa kupita kiasi
mzio – ugonjwa wa moyo na mishipa
- Jadili uhusiano uliopo kati ya mtindo wa maisha na magonjwa haya.
- Je, watu wengi wanaugua magonjwa haya katika nchi unazojua?
- Jadili sababu zinazoweza kupelekea wahamiaji kupata matatizo mengine ya kiafya kando na yale waliyokuwa nayo kabla ya kuja Norwe.
- Je, tunaweza kufanya nini kujiimarisha kiafya?
Ni msimu wa joto. Watoto watatu wa familia ya Hansen, wenye umri wa miaka saba, tisa na kumi na moja, wako nyumbani kwa ajili ya likizo baada ya kufunga shule. Wanaona siku hazisongi na zinawachosha. Marafiki wao wengi wako kwingine kwa sasa au wanafanya mambo mengine. Mama na baba huja nyumbani wakiwa wamechoka baada ya kazi na wakati hawapo kazini, wanataka kupumzika nyumbani. Kwa hivyo wakati mwingi familia hii huwa nyumbani.
- Je, unachukulia vipi hali ya familia hii?
- Unadhani wazazi wanapaswa kufikiria nini?
- Je, hali hii inaweza kuathiri afya ya watoto na wazazi?
- Je, hali hii inaweza kuathiri kitu kingine chochote kwa watoto?
Mehmet yuko darasa la sita. Ana marafiki wengi katika darasa lake. Wao hucheza sana kandanda wakati wa mapumziko. Marafiki zake wengi pia ni wachezaji katika timu ya soka ya eneo lao. Wao hufanya mazoezi wakati wa alasiri, mara mbili kwa wiki. Mehmet angependa kucheza katika timu hiyo lakini wazazi wake hawapendi wazo hilo. Inagharimu pesa, na familia haina pesa za kutosha.
- Je, hali hii inaweza kuathiri vipi afya ya Mehmet?
- Je, unachukulia vipi hali ya wazazi?
Chagua jibu sahihi
Je, hali ya maisha ikoje nchini Norwe hivi leo?
Kamilisha sentensi
Tunaweza kuimarisha afya kwa...
Chagua jibu sahihi
Ipi ni sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua picha sahihi
Je, ni picha zipi zinaonyesha mtindo wa maisha unaoimarisha afya? Unaweza kuchagua zaidi ya jibu moja.