Usawa
Tazama filamu
Usawa
Usawa kati ya watu ni mojawapo ya maadili muhimu zaidi katika jamii ya Wanorwe. Usawa inamaanisha kwamba tunaamini kuwa watu wote wana thamani sawa bila kujali jinsia, umri, nafasi zao, utamaduni, kabila au mwelekeo wa kimapenzi. Jamii inajitahidi kuwapa watu wote fursa sawa bila kujali uwezo wao binafsi. Mifano inajumuisha masomo kwa wanafunzi wenye matatizo mbalimbali, mafunzo ya lugha ya Kinorwe kwa wahamiaji, na kuwalipa wafanyakazi wote malipo sawa wanapofanya kazi inayolingana.
Katika miaka ya 1970, masuala ya haki za wanawake katika jamii, ajira na elimu ya wanawake yalianza kuangaziwa. Nafasi za ajira kwa wanawake zimeongezeka tangu wakati huo, na leo idadi ya wanawake walioajiriwa inakaribiana na ile ya wanaume. Hata hivyo, bado kuna kazi zinazochukuliwa kuwa za wanaume na zingine za wanawake. Ikilinganishwa na wanaume, wanawake zaidi hufanya kazi za muda. Takriban idadi sawa ya wanawake na wanaume sasa wana elimu ya juu, lakini chaguo zao za kitaaluma mara nyingi bado ni zilezile. Wanawake mara nyingi huchagua kozi katika taaluma za utunzaji na ualimu, nao wanaume hufanya kozi za teknolojia na sayansi. Japo idadi ya wanawake ni takriban nusu ya wafanyakazi wote, karibu wasimamizi wawili kati ya watatu bado ni wanaume.
Katika miongo iliyopita, tumeona mabadiliko ya mitazamo kuhusu majukumu ya wanaume na wanawake pamoja na nafasi zao katika umma, kwenye familia na nyumbani. Leo, familia nyingi hushirikiana katika utunzaji na kazi za nyumbani, haswa familia changa, lakini tafiti zinaonyesha kuwa wanawake bado hutumia wakati mwingi kufanya kazi za nyumbani kuliko wanaume. Ni wajibu wa kila familia kuamua jinsi ya kufanya shughuli na majukumu yao nyumbani. Hata hivyo, suala la usawa limejumuishwa katika sheria na haki. Kila mtu anayeishi Norwe lazima azingatie sheria hizi. Mifano ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Usawa na Kukabiliana na Ubaguzi, Sheria ya Ndoa na Sheria ya Urithi.
Kipengee cha 185 cha Sheria Jumla ya Adhabu ya Kiraia ya mwaka wa 2005 hujulikana kama aya kuhusu ubaguzi. Kifungu hiki kinapiga marufuku matamshi ya ubaguzi au ya chuki dhidi ya watu kwa misingi ya kabila, rangi ya ngozi, mitazamo yao, dini, mwelekeo wa kijinsia au ulemavu. Kifungu hiki kinawekea vikwazo uhuru wa watu katika kujieleza. Lengo la aya kuhusu ubaguzi ni kulinda makundi madogo ya watu.
Chanzo: SSB (Ofisi ya Takwimu ya Norway)
Jadilianeni pamoja
- Usawa haumaanishi tu usawa wa kijinsia. Unaweza pia kumaanisha usawa kati ya vizazi tofauti, watu wenye uwezo tofauti wa kifedha, watu wa mataifa na kabila tofauti, hali tofauti za ulemavu, dini, mwelekeo wa kijinsia nk. Jadilianeni pamoja kuhusu hili kwa mtu binafsi na jamii.
- Je, unadhani ni kwa nini vijana wengi zaidi ambao wazazi wao ni wahamiaji hufanya elimu ya juu ikilinganishwa na vijana ambao wazazi wao ni Wanorwe?
- Jadilianeni pamoja kuhusu sababu za wanaume na wanawake kufanya kazi mbali na nyumbani hivi leo nchini Norwe. Je, hii ina manufaa au athari zipi?
- Je, familia inawezaje kushirikiana licha ya kuwa mama na baba wanafanya kazi mbali na nyumbani?
- Ikilinganishwa na wanaume, wanawake zaidi wanafanya kazi za muda. Je, unadhani hii imesababishwa na nini? Je, hili linaathiri vipi mwanamke na familia kwa sasa na baadaye?
Kamilisha sentensi
Mojawapo ya maadili muhimu zaidi katika jamii ya Wanorwe ni...
Chagua jibu sahihi
Je, suala la haki za wanawake lilianza kuangaziwa lini?
Kamilisha sentensi
Japo idadi ya wanawake ni takriban nusu ya wafanyakazi wote, karibu...
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?