Huduma za afya
Huduma za afya
Katika nchi ambapo maslahi yanazingatiwa, lengo ni kuhakikisha watu wote wanaweza kuishi maisha mazuri kadri inavyowezekana. Hii inajumuisha kuwa wenye afya nzuri. Nchini Norwe, tuna huduma ya afya ya umma. Hii inamaanisha kwamba serikali inawajibika kuwapa watu huduma za matibabu wanazohitaji, bila kujali hali zao za kifedha. Huduma mbalimbali za afya zinapatikana pia. Wanaotumia huduma hizi hugharamia matibabu yao wenyewe.
Daktari wa familia
- Mpango wa daktari wa watu wote unamaanisha kuwa kila mtu anayeishi Norwe ana haki ya kuwa na daktari wa kawaida kama daktari wake wa familia. Ukiugua au mtoto wako akiwa mgonjwa, utawasiliana kwanza na daktari wako unayemtembelea mara kwa mara.
- Ikihitajika, daktari wako wa familia anaweza kukuelekeza kwa mtaalamu wa afya.
- Unapohitaji kumwona daktari wako maalum sharti umpigie simu na uweke miadi. Kawaida, unahitaji kusubiri siku chache kabla ya miadi, lakini unaweza kumwona daktari siku hiyohiyo ikiwa unajihisi mgonjwa sana.
- Unachagua daktari wako maalum. Unaweza kubadilisha daktari wako ikiwa hujaridhika, lakini si zaidi ya mara mbili kwa mwaka.
Kwenye tovuti ya helsenorge.no, unaweza kupata daktari wa kawaida, kubadilisha daktari na kupata maelezo mengine muhimu ya afya.
Mtandao
Mtaalamu wa afya
- Mtaalamu wa afya, kwa mfano, daktari wa magonjwa ya wanawake, daktari wa ngozi, daktari wa sikio, pua na koo au mtaalamu wa magonjwa ya watoto.
- Kwa kawaida, unapata rufaa kutoka kwa daktari wako ikiwa unahitaji kuona mtaalamu fulani wa afya.
Kulazwa hospitalini
- Daktari anaamua ikiwa unahitaji kulazwa hospitalini. Hulipishwi unapolazwa katika hospitali ya umma. Serikali italipia gharama zote za matibabu, chakula na malazi.
- Mtoto anapolazwa hospitalini, mzazi mmoja kawaida hukaa hospitalini ili kumshughulikia.
Matibabu kwa wagonjwa wasiolazwa hospitalini
- Matibabu ya kliniki/wagonjwa wasiolazwa inamaanisha kuwa unapokea matibabu hospitalini bila kulazwa. Unafika kwa miadi yako kisha unarudi nyumbani baada ya kupokea matibabu.
Huduma ya dharura
- Wewe au mtu katika familia yako akiugua au kujeruhiwa baada ya saa za kazi za daktari wako, unahitaji kuwasiliana na wodi ya dharura kwa kupiga simu kwa nambari 116 117.
- Ikiwa mtu ni mgonjwa sana au ameumia na anahitaji usaidizi wa haraka, unahitaji kupiga simu kwa nambari ya matibabu ya dharura, 113.
- Zungumza kwa utulivu na utoe habari kwa utaratibu ufuatao: Je, wewe ni nani? Nini kimetokea? Uko wapi?
Duka la dawa
- Dawa nyingi zinanunuliwa tu kwenye maduka ya dawa.
- Baadhi ya dawa, kama vile dawa za kupunguza maumivu, zinaweza pia kununuliwa kwenye maduka ya vyakula au kwenye vituo vya mafuta.
- Wanaofanya kazi kwenye maduka ya dawa wanaweza kukusaidia kuchagua dawa na watakuelezea jinsi ya kuitumia.
- Wakati mwingi unahitaji maelekezo ya daktari katika kununua dawa. Maelekezo hayo yanataja jina la dawa na jinsi ya kuitumia.
- Kawaida, maelekezo hutolewa kielektroniki na wakati mwingine huandikwa kwenye karatasi. Maduka yote ya dawa yanaweza kufikia maelekezo yaliyotolewa kidijitali.
- Sharti uweze kujitambulisha (kwa kutumia kadi ya benki, leseni ya dereva, pasipoti au kitambulisho) kwenye duka la dawa unapokwenda kuchukua dawa ulizopendekezewa.
- Endapo unaugua sana na una ugonjwa sugu, unaweza kupata dawa, bidhaa za lishe na vifaa vya kimatibabu utakavyolipia. Kisha unalipa kiasi kidogo cha gharama yote.
Wajibu wa usiri
- Watu wote wanaofanya kazi kwenye huduma ya afya wana jukumu la usiri. Hii inamaanisha kwamba hawawezi kushiriki na watu wengine maelezo yako binafsi bila idhini yako. Kwa hivyo unaweza kuzungumza wazi na daktari wako kuhusu matatizo yako. Hupaswi kuhofia kuwa mtu mwingine atajua ulichosema, ikijumuisha familia yako.
- Una haki ya kujua yale daktari anaandika kukuhusu kwenye rekodi yako ya matibabu.
- Wajibu wa usiri unadumishwa hata ikiwa mtu uliyezungumza naye atakwenda kufanya kazi kwingine.
- Wajibu wa usiri pia unahusisha wakalimani.
- Watoto waliofikisha umri wa miaka 16 wanaruhusiwa kuamua ikiwa wazazi wao wanaweza kupata maelezo yao ya afya.
Anacholipa mgonjwa
- Mgonjwa hulipa kiasi mahususi, nayo serikali hulipa salio la ada ya kumwona daktari.
- Wagonjwa hulipia bandeji, sindano, dawa, vipimo nk. Ada hizi hazijajumuishwa kwenye kiasi anacholipa mgonjwa kumwona daktari.
- Watoto walio chini ya miaka 16 hawalipi ada ya kumwona daktari.
Uchunguzi wa ujauzito haulipishwi. - Anacholipa mgonjwa anapokwenda kumwona daktari kwa miadi ya kawaida huwa kati ya NOK 150 na 300.
- Iwapo una ugonjwa sugu, unalipa ada ya kumwona daktari ili upate matibabu kupitia mpango wa "bluu" (ya kufidiwa).
- Baada ya kulipa kiasi fulani cha ada ya matibabu kwa mwaka, utaweza kupata kadi maalum ya matibabu (kadi ya "kutolipia huduma"). Ukilipa kiasi hiki kwa huduma za wagonjwa, Idara ya Usimamizi wa Masuala ya Afya (HELFO) itakutumia kadi ya kutolipia huduma, au utapata kadi hii kwa njia ya kidijitali kwenye helsenorge.no. Sharti ubebe kadi hii unapokwenda kumwona daktari au kununua dawa za kulipiwa. Hii inamaanisha kuwa huhitaji kulipia ada za mgonjwa kwa miezi iliyosalia mwaka huo.
Kuhusisha mkalimani
Ikiwa wewe na daktari hamuelewani, una haki ya kuhusisha mkalimani unapokwenda kumwona daktari. Hutalipia huduma hii.
Jadilianeni pamoja
- Je, huduma za afya ziko vipi katika nchi unazojua?
- Serikali hugharamikia matibabu ya wagonjwa. Je, serikali hupata pesa vipi?
- Je, faida ni zipi katika kuhudumiwa na daktari mahususi kila wakati?
- Je, kiko wapi chumba cha dharura kilicho karibu nawe?
Chagua jibu sahihi
Je, "huduma za afya ya umma" inamaanisha nini?
Chagua jibu sahihi
Je, unapaswa kuwasiliana na nani kwanza ikiwa unahitaji usaidizi wa daktari?
Chagua jibu sahihi
Je, mtu hulipa pesa ngapi kulazwa hospitalini nchini Norwe?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?