Mapato na ushuru
Mapato na ushuru
Mapato
Tunapozungumzia kuhusu mapato nchini Norwei, mara nyingi tunazungumza kuhusu mshahara wa kila mwaka au malipo ya kila saa. Malipo wastani ya kila mwaka nchini Norwei ni chini ya laki sita na sabini elfu za NOK kabla ya kodi (2023). Kwa wastani, wanawake wanapata mapato ya chini kuliko wanaume. Hii ni kwa sababu, kati ya sababu zingine, wanawake mara nyingi hufanya kazi za muda, na kuwa mara nyingi huchagua kazi za mapato ya chini.
Mapato yanaweza kujadiliwa. Majadiliano hayo hufanyika moja kwa moja kati ya mwajiri na mwajiriwa au kati ya wawakilishi wa mwajiri na wawakilishi wa wafanyakazi. Wafanyakazi wanapojiunga na chama cha wafanyakazi, chama hicho hujadili mapato kwa niaba ya wanachama wake.
Mishahara kawaida hulipwa kwenye akaunti ya benki mara moja kwa mwezi tarehe fulani. Mfanyakazi pia hupokea hati ya malipo inayoonyesha mapato pamoja na ushuru uliotozwa.
Chanzo: SSB (Ofisi ya Takwimu ya Norwe)
Ushuru
Nchi ya Norwe inategemea kabisa watu kulipa ushuru mbalimbali za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Miongoni mwa mambo mengine, ushuru huu hufadhili mfumo wetu wa maslahi. Wafanyakazi wote nchini Norwe hulipa ushuru kwa manispaa wanakoishi, na kwa serikali ya Norwe. Waajiri pia hulipa ushuru kwa manispaa na serikali.
Kila mtu anayepata zaidi ya kiwango kilichobainishwa kwa mwaka sharti alipe ushuru. Watu wote hawalipi kiwango sawa cha ushuru. Wenye mapato ya juu hulipa ushuru zaidi. Wenye mapato ya chini wanalipa ushuru kidogo. Inatekelezwa hivi ili wanaopata mapato zaidi wachangie zaidi kwa faida ya watu wote.
Unapoajiriwa, mwajiri wako sharti ajue kiasi cha ushuru anachohitajika kukutoza. Mamlaka ya Ushuru hukokotoa kiasi cha ushuru unachopaswa kulipa. Ni wajibu wako kuhakikisha kuwa maelezo yako yaliyo kwenye rekodi za Mamlaka ya Ushuru ni sahihi. Unaweza kuona na kubadilisha maelezo yako rasmi kwenye tovuti ya Mamlaka ya Ushuru. Mwajiri wako hupakua kadi yako ya ushuru.
Ni wajibu wa mwajiri kutoza ushuru kwenye mapato ya jumla ya wafanyakazi kabla ya kuwalipa. Mwajiri hutuma ushuru uliotozwa kwa mamlaka ya ushuru.
Fomu ya ushuru
Ushuru unaolipa hukokotolewa kulingana na maelezo yako kwenye Mamlaka ya Ushuru. Mwezi Machi/Aprili, kila mtu anapokea muhtasari wa mapato yake nk. kwa mwaka uliopita. Muhtasari huu ni wa kidijitali, na unahitaji kuingia kwenye www.skattetaten.no ili uangalie ripoti ya fedha. Ikiwa umelipa ushuru zaidi, utarejeshewa pesa. Ikiwa umelipa ushuru kidogo, utapokea ankara unayopaswa kulipa.
Mtandao
Mkataba wa ajira
Kila mtu anayeajiriwa anapaswa kupewa mkataba wa ajira. Mwajiri na mwajiriwa sharti watie saini mkataba. Sheria ya kazini inaelezea ni yepi yanapaswa kujumuishwa kwenye mkataba wa ajira. Miongoni mwa mambo mengine, sharti uwe na maelezo ya nafasi, malipo na saa za kazi.
Kufanya kazi kwa siri
Kufanya kazi kwa siri inamaanisha kufanya kazi bila mkataba na bila kulipa ushuru. Mwajiri halipi ada ya Bima ya Kitaifa ya mwajiri au ada nyingine ya Bima ya Kitaifa kwa ajili ya mfanyakazi. Kufanya kazi kwa siri ni hatia na kunachukuliwa kuwa uhalifu wa kiuchumi. Waajiri na wafanyakazi wote wanaweza kuchukuliwa hatua kutokana na Kufanya kazi kwa siri.
Kufanya kazi kwa siri pia ni kinyume na maadili. Wafanyakazi ambao hawalipi ushuru, hawachangii katika jamii. Kila mwaka, serikali ya Norwe hupoteza mamilioni ya pesa kupitia ushuru, ada za Bima ya Kitaifa kwa waajiri na ada za Bima ya Kitaifa kwa waajiriwa kutokana na wanaofanya kazi kwa siri. Hizi ni pesa ambazo zingesaidia kufadhili mfumo wa maslahi.
Kando na kuwa haramu na kinyume na maadili, kufanya kazi kwa siri kunaweza kumwathiri pakubwa mfanyakazi:
- kutolipwa anapokuwa mgonjwa
- kutolipwa anapokwenda likizo
- kukosa pensheni
- kutonufaika na faida zinazotolewa kwa wasio na ajira ukipoteza kazi
- kukosa bima ya ajali kazini
- kutoweza kupata mkopo wa benki
- hakuna mkataba wa ajira - hakuna marejeleo - hakuna ithibati ya uzoefu wa kazi - itakuwa vigumu kupata kazi nyingine
Jadilianeni pamoja
- Je, mfumo wa ushuru ukoje katika nchi yako?
- Je, mambo yangekuwa vipi Norwe watu wasipolipa ushuru?
- Kwa nini mkataba wa ajira ulioandikwa ni muhimu?
- Jadili athari za kufanya kazi kwa usiri, kwa mtu binafsi na jamii.
Chagua jibu sahihi
Je, mapato ya jumla ni nini?
Chagua jibu sahihi
Je, hati ya malipo ni nini?
Chagua jibu sahihi
Je, kufanya kazi kwa siri ni nini?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?