Siku muhimu na sikukuu za taifa
Siku muhimu na sikukuu za taifa
Mwaka Mpya
Siku ya kwanza ya mwaka ni tarehe 1 Januari. Inajulikana kama Mwaka Mpya. Shule hufungwa na hakuna kwenda kazini, watu wengi hupumzika siku hii.
Siku ya Kitaifa ya Wasami
Tarehe 6 Februari, Wasami nchini Ufini, Norwe, Urusi na Uswidi husherehekea Siku ya Kitaifa ya Wasami. Ni siku rasmi ya kupeperusha bendera, lakini sio sikukuu ya taifa.
Siku ya Wanawake
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa tarehe 8 Machi. Iliadhimishwa mara ya kwanza mnamo 1915. Katika miaka ya 1970, watu wengi walihusika katika kupigania usawa na haki za wanawake, na Siku ya Wanawake Duniani imeadhimishwa kila mwaka nchini Norwe tangu mnamo 1972. Watu hubeba mabango barabarani tarehe 8 Machi, na hotuba na taarifa hutolewa. tarehe 8 Machi sio sikukuu ya kitaifa.
Pasaka
Pasaka iko mwezi Machi au Aprili. Tarehe halisi hutofautiana kila mwaka. Pasaka ni sikukuu ya Kikristo inayoadhimishwa ili kukumbuka kifo na ufufuo wa Yesu Kristo. Kwa watu wengi wanaoishi Norwe, Pasaka sio hasa kuhusu dini, bali ni kipindi cha kupumzika siku chache baada ya msimu mrefu wa baridi.
Alhamisi Kuu, Ijumaa Njema na Jumapili ya Pasaka, na Jumatatu ya Pasaka ni sikukuu za kitaifa. Biashara hufungwa, na hakuna kwenda kazini sikukuu hizi. Wanafunzi huwa hawaendi shuleni wakati wa Pasaka, na wafanyakazi wengi huchukua likizo ya ziada pamoja na likizo ya kitaifa.
Pentekoste na Siku ya Kupaa kwa Yesu
Pentekoste na Siku ya Kupaa kwa Yesu ni sikukuu mbili za Kikristo. Siku ya Kupaa kwa Yesu ni Alhamisi siku 40 baada ya Pasaka, nayo Pentekoste huadhimishwa siku kumi baadaye. Pentekoste na Siku ya Kupaa kwa Yesu ni sikukuu za kitaifa kwa watu wengi, na hakuna kwenda kazini.
Siku ya Wafanyakazi
Siku ya Wafanyakazi Duniani huadhimishwa tarehe 1 Mei. Watu wengi hubeba mabango barabarani ili kutetea masuala ya kisiasa wanayounga mkono. Siku ya Wafanyakazi ni sikukuu ya kitaifa na hakuna kwenda kazini.
Siku ya Katiba
Siku ya kitaifa ya Norwe ni tarehe 17 Mei. Ni maadhimisho ya kutiwa saini kwa katiba ya Norwe mnamo tarehe 17 Mei 1814. Kwanza kabisa, Siku ya Katiba ni siku ya watoto. Karibu watoto wote wa chekechea na wanafunzi wengine huvaa mavazi maalum na kushiriki katika gwaride ambapo wanapeperusha bendera ya Norwe na kuimba. Bendi zilizovalia sare zenye rangi za kuvutia huongoza gwaride. Watoto wengi hucheza muziki katika bendi hizo.
Mara nyingi watoto huruhusiwa kula peremende na mkate wenye soseji kadri wanavyotaka. Watoto nchini Norwe hutazamia sana tarehe 17 Mei. Ni sikukuu ya kitaifa na hakuna kwenda shuleni.
Krismasi
Mwezi Desemba, watu wengi nchini Norwe husherehekea Krismasi. Krismasi ni sikukuu ya Kikristo ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Krismasi na sherehe za Krismasi ni utamaduni muhimu kwa watu wengi. Kimsingi ni sherehe ya familia.
Tarehe 24 Desemba inajulikana Mkesha wa Krismasi. Katika Mkesha wa Krismasi, ni kawaida kwa familia kula pamoja chajio cha jadi cha Krismasi. Sehemu mbalimbali za nchi zina utamaduni tofauti. Watu wengi wana mila zao binafsi ambazo wanachukuliwa kuwa muhimu kufuata. Ni kawaida kupeana zawadi kwenye Mkesha wa Krismasi – zawadi za Krismasi.
Siku ya kwanza na ya pili ya Krismasi ni sikukuu za kitaifa. Biashara hufungwa, na hakuna kwenda kazini sikukuu hizi. Wanafunzi huwaendi shuleni wakati wa Krismasi, na wafanyakazi wengi huchukua likizo ya ziada pamoja na likizo ya kitaifa.
Mwaka Mpya
Siku ya mwisho ya mwaka ni tarehe 31 Desemba. Siku hii inajulikana kama Mkesha wa Mwaka Mpya, na watu wengi huisherehekea pamoja na familia na marafiki. Usiku wa manane, tochi na fataki huangaza angani kwenye giza. Mkesha wa Mwaka Mpya sio sikukuu ya kitaifa.
Tamaduni na siku za kuadhimishwa zisizofuata kalenda: siku ya kuzaliwa, harusi, ubatizo, kipaimara na mazishi.
Jadilianeni pamoja
- Je, unafahamu siku zipi muhimu? Je, siku hizo muhimu husherehekewa vipi?
- Je, kwa nini watu husherehekea siku tofauti muhimu?
- Je, siku gani ni muhimu kwako? Je, kwa kuwa sasa unaishi Norwe, jinsi ulivyozoea kusherehekea siku hizo muhimu itabadilika vipi?
- Je, unadhani sikukuu nchini Norwe huenda zikawa muhimu kwako baada ya muda?
Chagua jibu sahihi
Je, ipi si sikukuu ya kitaifa?
Chagua jibu sahihi
Je, siku ya kitaifa ya Norwe ni lini?
Chagua jibu sahihi
Je, siku ipi ndiyo ya mwisho katika mwaka?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua picha sahihi
Je, siku ipi muhimu ni sikukuu ya kitaifa nchini Norwe?