Historia ya Norwe kuanzia 1814 hadi 1905
Historia ya Norwe kuanzia 1814 hadi 1905
Kuvunjwa kwa muungano na kuundwa kwa muungano mpya
Mwanzoni mwa karne ya 19 barani Ulaya kilikuwa kipindi cha vita kadhaa, ikiwemo vita kubwa iliyohusisha Uingereza upande mmoja na Ufaransa upande mwingine. Mgogoro huu unajulikana kama Vita vya Napoleon. Denmaki-Norwe walikuwa upande wa Ufaransa, na Ufaransa iliposhindwa katika vita, mfalme wa Denmaki alilazimika kuachilia Norwe itawaliwe na Uswidi, ambayo iliunga mkono Uingereza wakati wa vita.
Mnamo 1814, muungano kati ya Denmaki na Norwe ulivunjwa. Wanorwe wengi walikuwa na matarajio ya Norwe kupata uhuru, na wanaume 112 wenye usemi mkubwa walikutana Eidsvoll. Miongoni mwa mambo mengine, walitaka kuunda katiba ya Norwe huru. Mnamo Mei 17 mwaka huo, Norwe ilipitisha katiba yake, ndiyo maana 1814 ni mwaka muhimu katika historia ya Norwe.
Licha ya hayo, Norwe ililazimishwa kuingia katika muungano na Uswidi mnamo Novemba 1814. Muungano mpya na Uswidi ulikuwa huru zaidi kuliko muungano wa zamani na Denmaki. Norwe iliruhusiwa kuwa na katiba yake, kutekeleza mabadiliko kadhaa, na ilijitawala katika maswala ya ndani. Bunge la Norwe lilianzishwa mnamo 1814.
Sera za kigeni zilibuniwa na Uswidi, na mfalme alikuwa Mswidi. Aliitwa Karl Johan, na barabara kuu mjini Oslo ilipewa jina lake.
Uzalendo wa Kitaifa na utambulisho wa kitaifa wa Norwe
Vuguvugu la sanaa na utamaduni lilianzishwa Ulaya katikati ya karne ya 19. Lilijulikana kama Uzalendo wa Kitaifa. Ikawa muhimu kwa vuguvugu hili kuonyesha sifa tofauti za kitaifa, na mara nyingi ilitia chumvi kuhusu sifa hizi. Nchini Norwe, mkazo haswa uliwekwa kuhusiana na mandhari ya kuvutia ya nchi hiyo, na jamii za wakulima vijijini zilionekana kuwa kielelezo halisia cha Norwe. Uzalendo wa Kitaifa ulionyeshwa kupitia fasihi, uchoraji na muziki.
Watu wengi walizidi kujivunia kuwa Wanorwe, na watu wengi walitaka Norwe iwe nchi huru.
Baada ya kuungana na Denmaki kwa mamia ya miaka, lugha ya kuandikwa iliyotumiwa Norwe ilikuwa Kidenmaki. Kinorwe cha kuandikwa kinachojulikana sasa kama Bokmål ni lahaja ya Kinorwe inayotokana na Kidenmaki cha kuandikwa. Wakati wa enzi ya Uzalendo wa Kitaifa, Wanorwe wengi walihisi kwamba wanapaswa kuwa na lugha yao ya kuandikwa isiyotokana na Kidenmaki. Hiyo ikawa chanzo cha kazi ya mwanaisimu Ivar Aasen, ambaye alisafiri kote Norwe kukusanya mifano kutoka kwa lahaja tofauti za Kinorwe. Kutokana na mifano aliyokusanya, aliunda aina mpya ya Kinorwe cha kuandikwa: Nynorsk. Lugha ya Nynorsk na Bokmål zimebadilika sana tangu karne ya 19, lakini zote ni aina rasmi za Kinorwe kilichoandikwa. Lugha ya Kisami pia ndiyo lugha rasmi nchini Norwe.
Kutoka kilimo hadi viwandani
Norwe ilikuwa nchi iliyoendeleza kilimo. Katikati ya karne ya 19, karibu asilimia 70 ya watu nchini Norwe walikuwa wakiishi vijijini. Wengi wao walijitafutia riziki kupitia kilimo na uvuvi. Maisha yalikuwa magumu kwa watu wengi. Idadi ya watu iliongezeka, ardhi haikuwa ya kutosha na nafasi za kazi zilikuwa chache. Wakati huohuo, mabadiliko yalikuwa yakifanyika mijini. Viwanda vilianzishwa, na watu wengi walihama kutoka mashambani kwenda mjini kutafuta kazi. Maisha ya mjini yalikuwa magumu kwa familia nyingi za wafanyakazi. Watu walifanya kazi saa nyingi, na hali ya maisha ilikuwa duni. Familia mara nyingi zilikuwa na watoto wengi, na ilikuwa kawaida kwa familia kadhaa kuishi katika nyumba moja ndogo. Watoto wengi walilazimika kufanya kazi viwandani ili kusaidia familia zao kujikimu.
Kabla ya 1850, karibu asilimia 15 ya watu walikuwa wakiishi mijini. Kufikia mwisho wa karne ya 19, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi asilimia 35. Mnamo 1900, asilimia 23 ya walioajiriwa walikuwa wafanya kazi viwandani. Takriban Wanorwe laki nane walihamia Amerika kati ya mwaka wa 1850 na 1920.
Nchi huru na inayojitawala
Kufuatia makubaliano ya kisiasa na mfalme wa Uswidi, Bunge lilitangaza tarehe 7 Juni 1905 kwamba mfalme wa Uswidi si mfalme tena wa Norwe na kwamba muungano na Uswidi umekwisha. Hii iliibua hisia kali Uswidi na karibu isababishe vita kuzuka baina ya Norwe na Uswidi. Katika kura mbili za maoni zilizofanyika mwaka huo, iliamuliwa kwamba muungano na uswidi umefutiliwa mbali, na kwamba nchi mpya ya Norwe itakuwa ufalme.
Mfalme wa Uswidi alikubali matokeo ya kura hizi za maoni. Carl, Mwana wa Kifalme wa Denmaki, alichaguliwa kuwa mfalme mpya wa Norwe. Alichukua jina Haakon, jina la wafalme fulani wa zamani wa Norwe. Mfalme Haakon wa VII ndiye alikuwa mfalme wa Norwe kuanzia 1905 hadi alipofariki mnamo 1957.
Jadilianeni pamoja
- Je, kwa nini tarehe 17 Mei huadhimishwa nchini Norwe?
- Siku za kitaifa huadhimishwa kwa njia tofauti katika nchi mbalimbali. Siku ya kitaifa huadhimishwa vipi katika nchi unazozijua? Je, Norwe inalingana au inatofautiana vipi na nchi hizo katika kuadhimisha siku ya kitaifa?
- Wanorwe wengi waliendeleza hisia ya uzalendo wa kitaifa katika karne ya 19. Je, uzalendo wa kitaifa ni nini na huibuka vipi?
- Je, uzalendo wa kitaifa una manufaa au athari zipi?
- Je, unadhani muungano wa kale wa Norwe na Uswidi umeathiri kwa vyovyote vile uhusiano wa nchi hizi mbili hivi leo?
- Sasa umejifunza kuhusu historia ya Norwe kuanzia 1814 hadi 1905. Je, unafikiri ulichojifunza ni muhimu kwa maendeleo ya Norwe hivi leo?
Chagua jibu sahihi
Je, Norwe ilipata katiba yake lini?
Chagua jibu sahihi
Je, Norwe iliungana na Uswidi lini?
Chagua jibu sahihi
Je, Ivar Aasen aliunda vipi lahaja ya Nynorsk ?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Chagua taarifa sahihi au isiyo sahihi
Soma taarifa hizi. Ipi ni sahihi? Ipi si sahihi?
Bofya picha
Bofya mwaka sahihi. Je, Haakon wa VII alikuwa mfalme wa Norwe lini?